Our History


HISTORIA YA UPYAISHO KARISMATIKI KATOLIKI
SEHEMU YA KWANZA
SISTA ELENA GUERRA- MTANGULIZI WA UPYAISHO KARISMATIKI

Sala ya Papa Yohani XXIII
Wakatoliki wanaofuatilia historia ya mkondo wa UKK wanaamini kwamba upyaisho huu ni jibu la moja
kwa moja kutoka kwa Mungu la sala maarufu ya Baba Mtakatiu Yohani XXIII1 ya kuombea mataguso
mkuu wa pili wa Vatikano. Katika sala hiyo mwenye heri Yohani XXIII alimuomba Mungu afanyaye upya
muujiza wa Pentekoste katika kanisa la sasa. Hakuna chembe ya shaka, hakika upyaisho huu ni jibu la
hakika na la nguvu la Mungu kwa sala hiyo. Hata hivyo tunaporudi nyuma zaidi katika historia
tunagundua kwamba, kuna mtangulizi wa mbali zaidi wa UKK; sista Elena Guerra. Kwa kweli
tunapojifunza historia, tunagundua kwamba sista Elena Guerra si mtangulizi wa Upyaisho Karismatiki
Katoliki tu, bali mtangulizi wa Upyaisho Karismatiki kwa ujumla wake. Kuna sababu kuu mbili za
kumtangaza sista Elena kama mtangulizi halali wa Upyaisho Karismatiki Katoliki.

  1. Upo ushahidi wa kutosha kwamba sala ya Papa mwenyeheri Yohani XXIII na kiu yake ya kuona

Pentekoste mpya katika kanisa ina asili yake katika mawazo ya sista Elena Guerra. Kuna sababu
kuu mbili za kuthibitisha kwamba mawazo ya sista Elena Guerra yalichangia vikubwa katika
mawazo ya Yohani XXIII:
i. Siata Elena alisukumwa na kiu ya kutaka Upyaisho wa kanisa kwa kumrudia Roho
Mtakatifu. Kama utakavyoona, kiu hii pia ilikuwa ndani ya Papa Yohani XXIII.
ii. Kama vile kuthibitisha mwelekeo wake kwa sista Elena Guerra,miezi michache tu baada
ya kuchauliwa kwake kuwa Papa Yohani XXIII alimtangaza Sista Elena Guerra kuwa
Mwenyeheri akiwa mtu wa kwanza kutangazwa na Mwenyeheri na Yohani XXIII mwezi
April 1959. Miezi mitano baadaye Yohani XXIII alitangaza sala mashuhuri ya kuombea
1 Rejea: Pope John XIII, Humanae salutis,
September,1959
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
Mtaguso, kumwomba Mungu afanye upya miujiza yake katika kanisa kama Pentekoste
Mpya.
2. Kama tutakavyoona hapo mbele upo ushahidi wa kihistoria kwamba, mlipuko wa mkondo wa
Pentekoste2 ndani ya Ukristo mwanzo wa karne ya ishirini, kuna uhusiano wa moja kwa moja na
msukumo uliokuwa ndani ya sista Elena Guerra. Hili ni jambo litakaloonekana bayana kadiri
tunavyoendelea kujifunza historia hii.
Ufunuo Wa Kwanza
Siata Elena Guerra, ni mwanzilishi wa Shirika la Masista Waobleti wa Roho Mtakatifu, jumuiya ya
watawa wa kike ya kijimbo huko Lucca Italia. Kufikia mwaka 1885, sista Elena Guerra alikuwa tayari
anajulikana kama mtaalamu wa elimu na mwandishi wa vitabu vya kiroho. Wakati huo ndipo aliposikia
msukumo wandani wa kumuandikia barua Ppa Leo XIII kumwomba aliongoze kanisa kwenye upyaisho
kwa kumrudia Roho Mtakatifu. Lakini lakini alipomshirikisha ‘mtu mwema’ mmoja mawazo hayo,
alimshauri kwamba ni mawazo yasiyofaa kufikiriwa. Aliambiwa ni kiburi tu kinaweza kumfanya mtawa
kama yeye awazie kuandika barua kwa Papa.hivyo sista Elena akabaki na mawazo hayo kama siri yake
akisubiri siku zitakazofaa na akitarajia kupata mwanga zaidi juu ya mambo hayo.
Siku Zinazofaa Zaidi Na Mwanga Zaidi
Siku zianzofaa zaidi zilikuja miaka minane baadaye. Mwaka 1893, mpishi wa kike katika nyumba aliyoishi
sista Elena (wakati huo akiitwa Mama Elena, kwa heshima ya kuwa mwanzilishi na Mama Mkuu wa
shirika lake), kwa jina Erminia Giorgetti, alijisikia kuagizwa na Bwana amweleze Mama Elena mambo
ambayo Bwana anataka Mama Elena ayafanye. Mungu alimwagiza Erminia amwambie Mama Elena
kwamba lazima aandike barua kwa Papa kumwomba awaunganishe waumini wote katika maombi ya
kuendelea kwa Roho Mtakatifu ili arejeshe mioyo yote kwa Mungu. Erminia pia alitabiri kwamba Papa
angetoa waraka wa pekee kuhusu Roho Mtakatifu muda mfupi baada ya hapo.
Barua Kwa Papa Leo XIII
Mama Elena alimshirikisha mambo hayo kiongozi wake wa kiroho Askofu Giovanni Volpi ambaye
alimsaidia Mama Elena kupeleka barua 12 kwa Papa Leo XIII kati ya mwaka 1895 na 1903. Inaaminika
kwamba barua yake ya kwanza ndiyo iliyosababisha Papa Leo XIII aandike waraka wake Provida matris
caritate. Katika waraka huo, Papa aliagiza kanisa katoliki lote kusali novena kwa Roho Mtakatifu katika
kipindi cha siku tisa kabla ya siku ya Pentekoste.
Waraka Wa Papa Leo XIII
2 Maneno ‘Mkondo wa Pentekoste’ katika makala hii haitumiki kumaanisha makanisa ya Kipentekoste: bali
yanatumika kumaanisha mkondo mzima unoambatana na udhihirisho wa karama za Roho Mtakatifukama
ilivyokuwa katika Pentekoste ya kwanza (Mdo s.2), jambo ambalo ni urithi wa pamoja wa Ukristo wote.
3. ©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
Katika barua nyingine Mama Elena alimweleza Papa kwamba Mungu anataka waamini wpte waungane
katika sala isiyokoma kwa Roho wa Mungu,tena kuwe na vikundi vya sala vya kudumu duniani kote,
vinavyosali daima kwa Roho wa Mungu. Alimwambia Papa kwamba ingefaa sana kama sala ya ‘Uje Roho
Mtakatifu’ ingejulikana na kusaliwa na wengi kama ilivyo ‘Salamu Maria’. Mwaka 1897 Askofu Volpi
alirudi kutoka Roma ambako alionana na Papa akamuarifu Mama Elena kwamba Papa ameahidi kufanya
kila linalowezekana ili Roho Mtakatifuaenziwe. Muda mfupi baadaye mwaka huo, Papa akatoa waraka
wake Divinum illud munus, moja ya nyaraka bora sana za Roho Mtakatifu kutolewa na Papa yeyote.
Katika waraka huu, Papa alitamka wazi kwamba Roho Mtakatifu ndio tegemeo la kanisa kwa jamii,
familia na mtu binafsi. Alisema Roho Mtakatifu atleta umoja wa wakristo kati ya makanisa na uongofu
wa ilimwengu wote. Akaagiza tena kwamba kuwe na novena ya Roho Mtakatifu katika maparokia yote
katika siku tisa kbla ya siku kuu ya Pentekoste.
Papa Awahimiza Maaskofu
Ingawa maaskofu wengi walimshukuru Papa kwa waraka mzuri, inaonekana hawakutimiza maagizo
yake. Mama Elena akamwandikia Papa kwamba ‘ingekuwa heriwangetii kuliko kushukuru’! Pengine kwa
sababu ya baruua hii , Papa aliandika barua ya faragha kwa maaskofu akisikitika kwamba maaskofu
wengi walizingatia wito wake wa novena kwa Roho Mtakatiu kwa mwaka 1897 tu. Alisema ‘Baba
Mtakatifu anatunza tumaini la hakika kwamba maaskofu na wakleri wote kwa msaada wa Mungu
wataitikia jambo muhimu kma hili kwa bidii na ujasiri mwingi’.
Sala Ya Papa Leo XIII
Octoba 15, 1900, Mama Elena alipendekeza kwa Papa Leo XIII kwamba Papa afungue mwaka wa
kwanza wa karne mpya (1901) kwa kimba “Uje Roho Mtakatifu” kama sala ya kumwita Roho
Mtakatifu kwa jina la kanisa zima. Papa Leo XIII alifanya kama Mama Elena alivyoomba usiku wa
Desemba 31,1900 kuamkia Januari mosi 1901.
Mwanzo wa mkondo wa Pentekoste wa kisasa: Topeka, Kansas, Marekani.
Usiku huo huo, huko Topeka katika jimbo la Kansas, Marekani, mtu wa kwanza katika historia ya
mkondo wa Pentekoste wa kisasa alipokea Ubatizo Katika Roho Mtakatifu. Huko kulikuwa na shule ya
Biblia ikiitwa Bethel Bible School. Mchungaji Charles Parhamu alikuwa mkufunzi katika shule hiyo. Kwa
kipindi kilichotangulia siku hiyo, Mchungaji Charles na baadhi ya wanafunzi wake, walikuwa katika sala.
Nia yao kuu ilikuwa kupata mang’amuzi ya Roho Mtakatifu kamailivyokuwa kwa kanisa la kwanza, kama
linavyoonekana katika kitabu cha Matendo ya Mitume.
Usiku huo, mmoja wa wanafunzi wake wa kike jina lake Agnes Ozmanialimwomba Mchungaji Charles
amwekee mikono na kumwombea ili abatizwe katika Roho Mtakatifu. Mchungaji Charles akafanya kama
Agnes alivyoomba. Agnes alipokea Ubatizo Katika Roho Mtakatifu ukidhihirishwa na karama za kiroho
ambazo Mtakatifu Paulo anaziorodhesha katika 1Kor 12:4-11, ikiwa ni pamoja na karama isiyoeleweka
4
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
na wengi ya ‘kunena klwa lugha ngeni’. Tukio hili linaaminiwa na wana historia kuwa ndiyo mwanzo wa
mkondo wa Pentekoste wa kisasa.
SEHEMU YA PILI
KUJIFUNZA KUTOKA HISTORIA
Yako mambo mengi tunaweza kujifunza kutoka katika historia hii, kwa kuangalia matukio tofauti. Lakini
kuna matukio mawili ya pekee yaliyotokea usiku mmjoja; Sala ya Papa Leo XIII na Agnes Ozman
(mprotestanti) kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu. Inaonekana hapa kwamba Mungu amejibu sala ya
Papa kwa kutenda kwa Waprotestanti. Mwanafunzi mzuri wa historia hatafuti kupindisha historia ili
ifanane na matakwa yake, lakini anajaribu kijifunza kutoka historia maana ya matukio. Sisi tunajifunza
nini kutoka katika tukio hili la kihistoria? Kwa ufupi yako mawazo yapatayo sita tunayoweza kujifunza
kutoka katika historia hii:
i. Mawazo ya Mungu si mawazo yetu. (Isa 55:8,9)
ii. Mungu hana upendeleo. (Mdo 10:34).
iii. Kanisa la Mungu ni moja.
iv. Wakatoliki (Kanisa Katoliki) hawakuwa tayari hadi mwaka 1967.
v. Utendaji wa siri wa Roho Mtakatifu; ina maana kwamba kuna wakati wa Mungu kwa kila jambo
na utendaji tofauti kwa kila wakati (Mh 3:1-8).
vi. Roho huvuma atakako (Yn 3:8).
SEHEMU YA TATU
KUANZA KWA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE
Kutoka Topeka hadi Azusa na kusambaa
Hadi mwaka 1906 watu kadhaa huko Topeka walipokea ubatizo katika Roho Mtakatifu. Lakini jambo hili
halikusambaa haraka hadi mwaka 1906. Mwaka huo, William Seymour mhubiriwa madhehebu ya
Holiness alipokea mkondo huu kutoka kwa Mch. Charles Parham. William Seymour alipeleka ‘moto’ wa
Pentekoste huko Los Angeles, Califonia akianzia kwenye mtaa wa Azusa ambako kulitokea mlipuko
unaoitwa na wanahistoria wa mkondo huu ‘Uamsho wa Mtaa wa Azusa’. Kutoka hapo mkondo huu
ulienea Marekani kote ndani na nje.
5
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
Waumini wengi wa makanisa ya Kiprotestanti walipojaribu kuingiza mang’amuzi haya ya kipentekoste
katika makanisa yao ama walilazimishwa kuondoka kwenye madhehebu yao kwa kufukuzwa ama
walijiondoa wenyewe kwa kukata tama kutokana nakukataliwa na makanisa yao. Hao waliotoka
wakaanza makanisa tunayoita sasa makanisa ya Kipentekoste.
Kabla ya hapo kulikuwa na aina kuu mbili za makanisa ya kikristo: makanisa ya Kikatoliki na makanisa ya
Kiprotestanti. Lakini kuanzia hapo ukaanza mkondo mkubwa wa tatu ambao sasa unaonekana na
kutambulika wazi: Makanisa ya Kipentekoste. Hadi kufikia mwaka 1925 tayari kulikuwa na madhehebu
makubwa 38 ya Kipentekoste.
Chanzo cha Uhasama Kati ya Wapentekoste na Wakristo Wengine.
Shida moja kubwa ilijitokeza kutokana na kuanza kwa madhehebu ya kipentekoste, ni uhasama kati ya
madhehebu haya na madhehebu mengine. Kumbuka kwamba madhehebu haya yalianza kwa sababu ya
madhehebu menginekuwakataa watu waliopokea mang’amuzi ya kipentekoste. Watu watu walioanza
madhehebu haya pale mwanzo, hawakuanza kwa kupenda; lakini walianza kwa kukataliwa.
Kuna taarifa za waume hata wake waliowapeleka wenzi wao kwa madaktari wa akili, kwa sababu ya
kunena kwa lugha. Wazazi wengine walifanya hivyo kwa watoto wao. Zingatia kwamba hawa sio watu
waliokuwa na nia mbaya, bali ni watu waliowapenda ndugu zao na walitaka sana kuwasaidia ili
wasiharibikiwe zaidi.
Kwa upande mwingine wapentekoste nao hawakuwa na namna nyingine isipokuwa kuyaona makanisa
yale yaliyowakataa kama ni makanisa yanayompinga Kristo na hivyo wakaanza mafundisho yao ya
‘kujitenga na wasioamini’ wakimaanisha wale wa madhehebu yaliyowakataa.
Kutokana na haya ukuta ukawa umejengeka ambao ulimsaidia shetani peke yake.
Matatizo Yaliyosababishwa na Uhasama Huu.
Ukuta huu ulisababisha matatizo kadhaa yaliyojitokeza wakati Upyaisho Karismatiki ulipoanza katika
makanisa ya zamani.
· Ugumu wa makanisa kupokea Upyaisho Karismatiki:
Ilikuwa vigumu kwa makanisa ya zamani kuyapokea mang’amuzi ya kipentekoste.
· Ugumu wa Wapentekoste Kuukubali Upyaisho Karismatiki Katika Makanisa Mengine:
Ilikuwa pia vigumu kwa waumini wa makanisa ya kipentekoste kuwakubali waumini wa
madhehebu mengine waliopokea mang’amuzi ya kipentekoste kuwa kweli wamepokea karama
ileile waliyoipokea wao (Mdo 11:17).
· Wanaupyaisho Karismatiki Kuwaiga Wapentekoste:
6
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
Baadhi ya waumini wa makanisa ya zamani waliopokea Ubatizo katika Roho Mtakatifu (URM)
ingawa walipenda kubaki katika makanisa yao, walitaka sana kukubaliwa na waumini wa
madhehebu ya Kipentekoste. Ili wakubaliwe waliiga mambo mengi ya madhehebu ya
Kipentekoste ambayo kwa kweli ni mapokeo tu ya madhehebu hayo lakini si ya msingi hata
kidogo kwa kuendeleza Pentekoste Mpya katika makanisa yao.
· Wanaupyaisho Karismatiki Kupoteza Ubatizo Katika Roho Mtakatifu:
Bado kuna baadhi ya waumini wa makanisa ya zamani hasa Wakatoliki waliopokea Ubatizo
katika Roho Mtakatifu na kubaki katika makanisa yao, ili wakubalikeekama walivyotaka, hawa
waliacha baadhi ya mambo yanayoambatana na upyaisho Karismatiki kama vile karama ya
kunena kwa lugha ngeni na nyimbo za uchangamfu ambazo waliziona kuwa na za ‘Kipentekoste’.
SEHEMU YA NNE
MWANZO WA UPYAISHO KARISMATIKI (VUGUVUGU LA PENTEKOSTE KATIKA MAKANISA YA
KIPROTESTANTI)
Mkondo wa Pentekoste ulivunja ukuta na kuingia katika na kuingia katika makanisa ya
kiprotestanti. Mwaka 1960 Mchungaji Dennis Bennet aliyakuwa Mchungaji kiongozi wa Parokia
ya Mt. Marko ya kanisa la Episkopo huko Van Nuys, Califonia , Marekani, alipokea Ubatizo wa
Roho Mtakatifu wakati akisali pamoja na rafiki zake. Baada ya hapo Mch. Dennis aliweza kujenga
kikundi cha sala cha watu kama 70 ndani ya Parokia hiyo ingawa haikuwa jambo rahisi.
Kuanzia hapo mkondo huu ukaenea katika makanisa ya kiprotestanti. Mwezi Agusti,1961 Mch.
Larry Christenson, wa kanisa la Kiluteri la sinodi ya amerika alipokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Larry aliwakusanya wachungaji wenzake 60 akamwalika (Mch. David du Plessis, mmoja wa
wapentekoste wa kwanza kukubali mkondo wa Pentekoste ndani ya makanisa ya zamani)
awahutubie, baada ya hapo mkondo huu ukashika moto kati ya waprotestanti.
SEHEMU YA TANO
UPYAISHO KARISMATIKI KATIKA KANISA KATOLIKI
Utangulizi.
Mwaka 1967 mkondo wa Pentekoste sasa ukiitwa upyaisho Karismatiki, ulivunja ukuta
usiotarajiwa kupita kuta zote; uliingia katika kanisa Katoliki. Wakatoliki hawakutarajia kama
‘upuuzi’ uliokubaliwa na waprotestanti, ungeingia ndani ya kanisa lao kongwe Takatifu.
7
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
Walijiona kama ni ngome imara ya kale isiyoweza kupenyeka, lakini hilo halikuweza kumzuia
Roho Mtakatifu kuangusha ukuta wa ‘Yeriko’!
Wengine nao, hasa wapentekoste walio wengi , hawakutarajia kwamba Roho Mtakatifu ‘wao’
katika Utakatifu wake angekubali kuingia kwa watu wagumu kama wakatoliki. Yote haya
hayakumzuia Roho Mtakatifu kuwashangaza hawa na hata wale wa kwanza. Upyaisho
Karismatiki ukawa umetinga katika kanisa Katoliki; ndiko kuzaliwa kwa upyaisho Karismatiki
Katoliki (UKK) au kwa lugha ya kiingereza Catholic Charismatic Renewal (CCR).
Papa Yohani XXIII
Ingawa UKK ilizaliwa kweli mwaka 1967, tulio wengi tunafuatilia historia yake ya karibu, kadiri ya
miaka tisa nyuma ya mwaka huo. Mwaka 1958, Papa Pio XII alifariki. Bila kutarajiwa na
ulimwengu, mzee, Angelo Kardinali Roncali alichaguliwa kuwa Papa akachagua jina la Yohani
XXIII. Wengi walimtazama kama papa wa mpito, atakayeishi miaka michache, bila kufanya
lolote la pekee, ili Kanisa lipate nafasi ya kupata Papa mwingine. Lakini Papa Mwenyeheri Yohani
XXIII mwenyewe hakujitazama hivyo. Alijitambua kama mtu aliyepewa kazi na Mungu ambayo
lazima atimize sehemu yake na kuwaachia watakaomfuata sehemu yao.
Papa Yohani XXIII atangaza Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano- Januari, 1959.
Januari 25, 1959, siku ya kuongoka kwa Mtume Paulo, Yohani XXIII aliitisha Mtaguso Mkuu wa
Pili wa Vatikano, mbele ya jopo tukufu la Makardinali. Wote waliodhani Yohani angekuwa Papa
wa mpito tu bila kufanya lolote la pekee, walishangazwa.
Sista Elena Guerra atangazwa Mwenyeheri- April 1959
Aprili 26, 1959 Papa alimtangaza Mama Elene Guerra kuwa Mwenyeheri akimwita ‘Mtume wa
Roho Mtakatifu’ na kutamka kwamba: ‘…ujumbe wake (Elena) ni wa maana kwa nyakati zote’.
Mara kwa mara Yohani XXIII alirudia wito wa Elena wa kuwa na Pentekoste Mpya.
Sala ya Yohani XXIII – Aprili, 1959
Mwaka huo mwezi Septemba, Yohani alitangaza sala ambayo aliagiza wakatoliki wote wasali ili
kuombea Mtaguso. Katika sala hii alimwomba Mungu hivi: “Fanya upya maajabu yako katika
siku zetu hizi kama kwa Pentekoste mpya”. Papa Mwenyeheri Yohani alitaka Mtaguso uwe
nafasi ya kanisa kupokea Pentekoste mpya.
Kufunguliwa na Kuanza kwa Mtaguso
Baada ya maandalizi ya miaka mitatu, Oktoba 11, 1962, Papa Yohani XXIII alifungua rasmi
Mtaguso. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Papa alidokeza kwamba, kuitisha kwake Mtaguso
kulitokana na uvuvio wa pekee wa kutoka kwa Mungu. Alisema, “Ilikuwa ni kuguswa kama kwa
ghafla: mwali wa utokao juu: utamu mkubwa machoni na moyoni”. Mtaguso uliendelea kwa
8
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
miaka maitatu hadi 1965 ingawa yeye mwenyewe alifariki katikati ya Mtaguso Juni 3, 1963 na
Paulo VI kuchukua nafasi yake. Mtaguso ulitoa jumla ya hati 16.
Leo Kardinali Suenens
Moja ya mambo yaliyoleta mjadala mkali ndani ya mtaguso ni suala la Roho Mtakatifu huku
baadhi wakisema kanisa limekua na kujijenga kwa hiyo karama za Roho Mtakatifu hazihitajiki
tena. Lakini Leo Kardinali Suenens alisimama na hoja nzito kupinga hoja hii akisema kwamba
Karama za Roho Mtakatifu ni za vizazi vyote na kwa waumini wote bila kubagua.
Hoja ya kardinali Suenens ilishinda na hivyo mtaguso ukatoa tamko linalochukuliwa na wengi
kuwa ni kuruhusu Upyaisho Karismatiki Katoliki. Kardinali Suenens ambaye alitumiwa na Mungu
kutetea hoja hii katika Mtaguso, ndiye Kardinali wa kwanza wa kanisa Katoliki kupokea binafsi na
kutetea hadharani Upyaisho Karismatiki Katoliki.
Mwisho wa juma la Dukeni
Mtaguso ulifungwa rasmi na Papa Paulo VI Desemba 8, 1965. Tayari wakati huo cheche za
upyaisho zilikuwa zimeanza kuonekana kati ya wakatoliki wengi. Miaka hiyo ambayo
mporomoko mkubwa wa maadili, ilishuhudia pia kiu kubwa ya mambo ya kiroho katika jamii.
Tukio linalohesabiwa na wengi kuwa ni mwanzo wa Upyaisho Karismatiki Katoliki, ni tukio
linaloitwa kwa kiingereza ‘Duquesne Weekend’ (Mwisho wa Juma wa Dukeni). Hakika yako
matukio mengine ya mlipuko huu yaliyotoke wakati huo huo lakini tukio la Dukeni ndilo
lililoandikwa zaidi kuliko mengine.
Tukio la mwisho wa juma la Dukeni lilitokea hivi.
Kikundi cha wakufunzi walei wa Chuo Kikuu cha Dukeni kinachoendeshwa na Mapadre wa
Shirika la Roho Mtakatifu (Duquesne University of the Holy Spirit), huko Pittsburgh, Marekani,
walianza kukutana kwa miezi kadhaa wakijaribu kutafakari kile kinachopungua katika maisha yao
binafsi. Hatimaye hawa hatimaye hawa walivutiwa kuhudhuria mkutano wa sala wa Upyaisho
Karismatiki uliokuwa ukiendeshwa na Waepiskopali katika eneo lao kama namna ya kujifunza.
Wawili kati yao walirudi kwenye mkutano huo juma moja baadaye na wakabatizwa katika Roho
Mtakatifu. Hawa wawili walikuwa mwanzo wa Ubatizo wa Roho mtakatifu (URM) kuwafikia
watu kadhaa hapo chuoni. Hatimaye wale waliopokea URM waliwaalika wengine wachache,
wengi wao wakiwa vijana wanafunzi katika mafungo ya mwisho wa juma (Februari 17-18,1967)
kwa lengo la kuwaombea Ubatizo katika Roho Mtakatifu. Hili ndilo tukio maarufu la mwisho wa
juma wa Dukeni.
9
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
Wale vijana wote wakabatizwa katika Roho Mtakatifu. Mmoja wao ni Patricia Galagher
Mansfield ambaye ambaye ameueleza ushuhuda wake mahali pengi. Ushuhuda huo sasa
umetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na jumuiya ya Agape, Dar es Salaam. Mwezi mmoja
baadaye Machi, 1967, Ralph Martin, Steve Clark, Gerry Rauch na Jim Carvanar ambao walikuwa
viongozi wa kitaifa wa Kursilo(vugu vugu la kiroho), walitembelea Dukeni. Huko walikuta moto
umeanza na wao pia wakabatizwa katika Roho Mtakatifu. Baadaye hawa wane walirejea vituoni
kwao kwenye vyuo vikuu vya Michigan na Notre Dame ambako walisambaza mota na hivyo
Upyaisho Karismatiki Katoliki(UKK) ukaanza kuenea. UKK ulienea kwa kasi sana Marekani kote na
nje ya Marekani. Miaka minane baadaye Ralph Martin mmoja wa viongozi wa mwanzo kabisa
wa Upyaisho Karismatiki Katoliki aliarifu kwamba Upyaisho Karismatiki Katoliki sasa umeenea
karibu katika kila nchi duniani.
Kupokelewa na Vatikano
Mwezi Octoba 1973, Papa Paulo VI alifanya mkutano wa pekee na vionngozi 13 walioshiriki
mkutano wa kimataifa wa viongozi wa Upyaisho Karismatiki Katoliki mjini Roma. Katika mkutano
huu Papa alisema maneno ya kutia moyo UKK. Katika mikutano na viongozi wa UKK , mapapa
Paulo VI na Yohani Paulo II, wameendelea kutia moyo na kufurahia utendaji wa UKK. Mwanzoni
mwa miaka ya sabini Papa Paulo VI alimuomba Leo Kardinali Suenens achukue jukumu la
kichungaji kwa UKK.
Mwaka 1993, hati maalumu ya kanisa ilitolewa nakatika kutambuliwa huko jina rasmi
likabadilishwa na kuwa ‘Huduma ya Kimataifa ya Upyaisho Karismatiki Katoliki’ (International
Catholic Charismatic Renewal Services – ICCRS).
Upyaisho Karismatiki Katoliki kote duniani hadi Tanzania
Hadi sasa UKKK umepokewa karibu katika nchi zote za dunia. Hapa Tanzania vikundi vya sala
vimeenea katika parokia nyingi kwa idhini ya maparoko na katika majimbo mengi maaskofu
wameonyesha ushirikiano , ukaribisho mkubwa na nia nzuri ya kutaka kusaidia kulea vuguvugu
hili. Wapo pia maaskofu kadhaa ambao wamepokea rasmi UKK katika majimbo yao na wengine
kuteua walezi.
Ili kuwa kama chombo kinachowaunganisha wakatoliki wanoshiriki UKK hapa Tanzania, na ili
kuendeleza mawasiliano bora na viongozi wa kanisa, kuna ‘Kamati ya Huduma ya Upyaisho
Karismatiki Katoliki Iliyoko Tanzania’ (UKKIT). Kamati hii inajumuisha viongoziwalei kutoka
majimbo ambamo UKK imeruhusiwa na maaskofu wake na pia mapadre au watawa walioteuliwa
na maaskofu wao kwa ajili ya kulea vikundi vya sala katika majimbo husika.
Sehemu hii ya historia ya Upyaisho Karismatiki Katoliki imetolewa na
Kamati ya viongozi wa Karismatiki Katoliki Parokia ya Chuo Kikuu Dar es Salaam
10
©Catholic Charismatic Renewal UDSM 2010
imenukuliwa kutoka katika kitabu cha
Semina Za Maisha Ya Kiroho
Masomo ya Walimu
Kilichoandikwa na Dr. Alex Victor Lengeju